Tuesday, January 21, 2014

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUWA MSHINDI DHIDI YA DHAMBI NA MABAYA YA AINA YOYOTE (IMPORTANT THINGS WHICH YOUR REQUIRED TO DO IN ORDER TO WINER ABOUT SINS)


MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUWA MSHINDI DHIDI YA DHAMBI NA MABAYA YA AINA YOYOTE (IMPORTANT THINGS WHICH YOUR REQUIRED TO DO IN ORDER TO WINER ABOUT SINS)  BY WILLY

 

Ndugu  yangu mpendwa tunakusalimu katika jina la Bwana Yesu Kristo. Mimi na familia yangu hatujambo kabisa tunamshukuru Mungu ambaye ameendelea kututunza na kutuvusha mwaka 2012 na kutuingiza mwaka huu wa 2013. Mwaka uliopita kwetu sisi ulikuwa ni mwaka wenye mafanikio mengi sana. Kwa kweli Bwana alitutnza na kutufanikisha kwenye mambo mengi sana, kiafya, kiuchumi, kihuduma tumemuona Mungu akitustawisha. Mwaka jana tumekutana na changamoto nyingi sana pia. Tulimpoteza baba yetu mpendwa Mzee Seth Mwang'onda. Baba yake mke wangu. Tuliwapoteza ndugu zetu wengi sana wa karibu. Lakini tunamshukuru Mungu atufarijiaye na kututia nguvu. Na amini hata wewe mwaka jana Mungu amekufanikisha sana, na hata ulipokwama mwamini Mungu kukutendea mema mwaka huu. Pia tunahitaji sana maombi yako mpendwa. Kwani tuna ratiba ndefu sana mwaka huu, tuombee kwa Mungu ili tufanikiwe sana katika mipango yetu yote. Pia tunahitaji michango yenu mbalimbali. Unaweza kuingia kwenye eneo la kuchangia huduma katika tovuti hii na ukapata maelezo. Ebu tusonge mbele tena na kuziangalia salamu za mwezi huu wa Kwanza kabisa katika mwaka huu wa 2013.  Kumbuka Tumekuwa na salamu zenye kichwa 

 

MAMBO MUHIMU UNAYOTAKIWA UYAFANYE ILI UPATE KUWA MSHINDI DHIDI YA DHAMBI NA MABAYA YA AINA YOYOTE. (SEHEMU YA KWANZA). Neno la Mungu linasema hivi  

 

“Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa ; nayo yatufundisha  kukataa ubaya na tamaa za kidunia;...(Tito 2:11).

 

Kila mtu aliyeupokea wokovu lazima ajifunze namna ya kuukataa ubaya na tamaa za kidunia. Ndiyo maana Mungu imempendeza kuweka neno lake ndani yangu ili kila mtu aliyeokoka ampate kujifunza mbinu za kuukataa ubaya na tamaa za kidunia. Katika salamu zilizopita tulianza kuliangalia eneo la MILANGO YA LAANA. Tulianza kuangalia mlango wa kwanza nao ni ule wa kutokuwaheshimu baba na mama. Mwezi huu tuaangalie mlango mwingine unaoweza kupitisha laana kwako wewe na hata katika uzao wako.

 

MLANGO WAPILI: KUTOKUTOA SADAKA NA UCHOYO 

 

Watu wengi waliookoka hujiuliza swali hili. Hivi inawezekana mtu aliyeokoka akapatwa na laana? Na wengine hawajui neno laana maana yake nini. Neno laana maana yake halisi ni nguvu inayozuia mafanikio ya mtu. Yawe mafanikio ya kiroho, kiafya, kiuchumi, kiakili nk. Sasa ngoja nijibu swali hilo. Ni ndiyo. Upo uwezekano kabisa ukawa umeokoka kabisaa lakini ukajikuta umekaliwa na mabaya hayo ya kutokufanikiwa.  Moja ya mlango ambao unawezakupitisha laana katika maisha yako na uzao wako ni huu wa kutokutii agizo la Mungu la kutoa sadaka na ukarimu.

 

Watoto wa Mungu wengi hukimbilia kuomba maombi mengi sana. Wengi hufunga na kuomba sana Mungu awabariki, lakini wanajikuta kila wanapomaliza maombi yao ndiyo wanazidi kukwama. Wengi hufikria ni adui amezuia baraka zao. Hufanya maombi ya kukemea roho zinazozuia mafanikio yao. Lakini wanapomaliza maombi hayo ya kukemea ndipo hukwama zaidi. Wengi hukimbilia kusema ni majaribu mpendwa. Au utawasikia wakisema ni vita mpendwa! Sikiliza ndugu yangu ikiwa leo hii wewe hutoi sadaka, na ukitoa unatoa sadaka kilema, Mungu anakulaani. Angalia maneno haya ya Bwana Mungu jinsi yasemavyo.

 

“Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake;basi, kama mimi ni baba yenu heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni Bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi  mwasema, tumelidharau jina lako kwa jinsi gani? Mnatoa  chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu. Nanyi mwasema, sisi tumekutia unajisi kwa jinsi gani? Kwa sababu mwasema, Meza ya Bwana ni kitu cha kudharauliwa. Tena mtoapo sadaka aliyekipofu, si vibaya!na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya! Haya! Mtolee liwali wako; je!atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema Bwana wa majeshi?......... tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatika kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je! Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana. Lakini na alaaniwe mtu mwenye kudanganya, ambaye katika kundi lake ana mume, akaweka nadhiri, ila amtolea Bwana kitu kilicho na kilema; kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika mataifa.” (Malaki 1:6-14).

 

Ukiyaangalia maneno hayo utagundua kuwa Mungu amesema wazi kuhusu habari ya kuwalaani watu ambao hawamuheshimu. Mungu anazungumza na makuhani, hazungumzi na wapagani. Unajua katika agano jipya kuhani ni mtu gani? Katika Agano Jipya kila mtu ambaye amemwamini Yesu na kumpokea Mungu amempa nafasi ya kuwa kuhani. Sasa sikiliza kuhani wewe. Mungu anasema wazi kuwa ikiwa hautoi sadaka kwa uzuri fahamu atakulaani. Mungu anaikataa sadaka isiyo kamili yeye ameiita sadaka kilema. Kwa lugha nzuri sadaka dhaifu. Fikiria una shilingi laki moja  ya matumizi yako ya kawaida kabisa, na unapewa  nafasi kanisani ya kumtolea Mungu angalia unavyotoa. Unatoa mia tano. Ungekuwa wewe ndiyo umefanyiwa tendo hilo ungefanya nini? Watu wengi watoapo sadaka wanatoa vitu dhaifu, ngoja nikupe mfano. Zaka ya shiringi elfu kumi ni shilingi elfu moja. Wewe unatoa shilingi mia nane. Mungu anakuona umetoa sadaka kilema. Hiyo ni sadaka isiyokamili

 

Na anasema kuwa watu hao walisema jambo hilo limetuchokesha. Ndivyo ilivyo kwa Wakristo wengi. Wanaposikia habari za sadaka, wengi husema hivyohivyo. Kama wewe ni mtu wa tabia hiyo Mungu anasema umelaaniwa kwa laana. Angalia maneno haya katika kitabu cha (Malaki 2:1-4).

 

“Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitu kuza jina langu. Asema Bwana wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana. Nami nitazilaani baraka zenu; naama nimekwisha kuzilaani. Kwa sababu hamyatii haya moyoni. Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo.”

 

Mungu anasema wazi kuwa ikiwa hatutayatia moyoni maagizo yake ya kutoa sadaka, basi atakachokifanya ni kutulaani. Anasema atapaka mavi katika sura yako. Ebu fikiria ni Wakristo wangapi ambao hawatoi sadaka vizuri na leo hii wanatafuta mpenyo wa kupenya katika suala la mafanikio yao lakini wamekwama? Ni wengi mno. Sikiliza mpendwa leo hii jambo baya sana la kutokufanikiwa kiuchumi limewakalia watu wengi sana, kisa ni laana inayotokana na kutokutoa sadaka, watu wengi hawatoi sadaka ila wanataka baraka. Hata watumishi wa Mungu wengi wamejikuta wamekwama kisa ni hikihiki cha kutokutoa sadaka. Sikiliza mtumishi unatakiwa ujifunze kumtolea Mungu sadaka. Neno la Mungu linatufundisha kuwa Mungu aliwaagiza Walawi na hata Makuhani  wahakikishe wanatoa sadaka. Angalia maneno haya ya Bwana jinsi yasemavyo.

 

“Bwana akanena na Musa na kumwambia, matoleo ya Haruni na wanawe watakayo mtolea Bwana , katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya;.....” (Mambo ya Walawi 6:19-23).Angalia na mistari hii. “Kisha Bwana akanena na Musa na kumwambia. Tena utanena na Walawi na kuwaambia  hapo mtakapoitwaa zaka  mkononi mwa wana wa Israeli, niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi  wenu, ndipo mtakaposogeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana  katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka. Na sadaka yenu ya kuinuliwa itahesabiwa kwenu kama ndiyo nafaka ya sakafu ya kupuria, na kama kujaa kwake kinu cha kushindikia zabibu. Hivyo ninyi nanyi mtasogeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika zaka zenu zote. Mpokeazo mikononi mwa Israeli; kwa hiyo mtampa Haruni kuhani hiyo sadaka ya kuinuliwa  kwa Bwana.....”(Hesabu 18:25-32).

 

Mungu anatufundisha kupitia maneno hayo wazi kuwa hata watumishi walitakiwa wajifunze kutoa sadaka.

 

Kwa nini leo hii watumishi wengi ni masikini sana? Jibu lake ni hili, angalia utoaji wao wa sadaka. ndipo utakapo ona kinachowazuia wasifanikiwe kiuchumi.  Watumishi walitakiwa kutoa zaka na matoleo mbalimbali ili na wao wapate kubarikiwa na Bwana. Lskini watumishi wengi hawatoi sadaka. Kutokana na kutotii maagizo hayo ya Bwana katika kona hii ya kutoa sadaka, ndio maana utaona watoto wa Mungu wengi hawafanikiwi kiroho, kiafya, kiuchumi nk.

 

Ndugu jifunze kuwa mkalimu, ndipo utapoepukana na jambo baya la laana. Sikiliza Bwana Yesu anatufundisha wazi kuwa lazima tuwape watu vitu ndipo nasi tutakapopewa vitu. Angalia maneno ya Bwana Yesu Kristo.

 

“Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika. Ndicho watu watakachowapa vifuanimwenu. Kwa kuwa kipimo kilekile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” (Luka6:38).

 

Kama unataka leo mafanikio lazima ujifunze kuwa mkarimu kwa watu na kwa Mungu pia. Angalia namna watoto wa Mungu wengi tulivyo. Utaona tumejaa ubinafsi mwingi sana. Mungu atusamehe na kutuondolea laana. Fikiria namna watu wengi wanavyotaka kupewa vitu mbalimbali kwa wingi, wakati wao hawataki kutoa vitu kwa watu. Hivyo ndivyo tulivyo. Badilika mpendwa ili utoke kwenye laana iliyokukalia. Sikiliza mpendwa Bwana anakupenda sana ndiyo maana leo hii ana kupatia ujumbe huu mzuri ili ubadilike  kutoka kwenye tabia hiyo mbaya ya uchoyo. Siku moja Mungu alinifundisha faida ya ukalimu. Ona mfano huu wa namna Mungu alivyompa Ibrahimu mtoto. Neno la Mungu linasema, Ibrahimu aliwakaribisha nyumbani kwake watu watatu. Walipokaa hapo ndani na kula chakula, ndipo Bwana alipomwambia Ibrahimu kuwa Sara atakuwa na mtoto wakati kama huo mwakani. Fikiria kama Ibrahimu asingewapokea  wageni hao ambao walikuwa ni malaika wawili  na Bwana Mungu mwenywe.

 

Na amini kuwa asingelikuwa mkalimu muujiza wake ungelimpita hivi hivi. Soma Kitabu chote cha (Mwanzo18:1-15) utaiona habari hiyo nzuri ninayokuambia. Sehemu nyingine neno la Mungu linatupa akili likisema hivi.

 

“Msisahau kuwafadhili wageni  maana kwa njia  hii  wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.” (Waebrania13:2)

 

Fikiria leo hii umemkilimu malaika wa Bwana alipokuja nyumbani kwako, unafikiri Mungu atakufanyia nini? Na amini Mungu atakubariki sana. Ebu tumalizie salamu hizi za mwezi huu mpya wa kwanza kabisa kwa mwaka huu wa 2013 kwa kujifunza kuwa watoto wakalimu na watoaji sadaka njema kwa Mungu ili tufunguliwe kutoka katika mkandamizo wa laana.  Nakushauri jipange moyoni mwako kwa kujiwekea malengo maalumu kwa kujitoa zaidi katika kuhakikisha unafadhiri kazi ya Mungu kwa mali zako, jiwekee malengo ya kuwatunza watumishi wa Mungu na hata kuwafadhiri watu ili Mungu akufungulie mlango wa baraka nyingi kwa mwaka huu wa 2013. Mungu akubariki sana

 

 

BY EVENGEILIST

 

WILLY M. SAMLEGA

No comments:

Post a Comment